Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, amewataka waumini kuendeleza utamaduni wa kukusanyika kwa ajili ya Dua, akisisitiza kuwa mshikamano na dua ni nguzo muhimu za kudumisha Amani, Upendo na Umoja katika Jamii.

21 Julai 2026 - 08:25

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, jana alifanya ziara katika Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Rufiji, ambapo alihudhuria dua ya kuwaombea waliotangulia mbele ya haki katika familia ya Alhaji Hajji Mageni Mnyonge, aliyefiwa na mama yake takribani mwezi mmoja uliopita.

Katika dua hiyo, Sheikh Jalala aliwahimiza waumini kuendeleza utamaduni wa kukusanyika kwa ajili ya dua na kumuomba Mwenyezi Mungu, akieleza kuwa utaratibu huo ni sehemu ya urithi wa wanazuoni na masheikh waliotangulia, ambao walikuwa wakikusanyika katika mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu bila kujali tofauti za kiitikadi.

Sambamba na hilo, Sheikh Jalala alisisitiza kuwa dua na mshikamano ni miongoni mwa nguzo muhimu za kudumisha amani, upendo na umoja katika jamii.

Aidha, aliwataka wakazi wa Ikwiriri kuendelea kuishi kwa maelewano, kuheshimiana na kushirikiana katika kulinda na kuhifadhi amani ya kijiji chao.

Sheikh Jalala amekuwa akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa umoja, mshikamano na kuheshimiana miongoni mwa wananchi, akieleza kuwa jamii yenye mshikamano na inayoshirikiana katika mambo ya kheri inaweza kujenga mazingira ya amani, upendo na maendeleo kwa wote.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha